Tuesday, 17 February 2009

Pinda kulia hakutoshi, awajibike



INGAWA kilio cha Waziri Mkuu, Mizengo Peter Kayanza Pinda, kinaonekana kuyeyusha hasira za Watanzania kwa muda, kuna haja ya kudodosa zaidi.

Wapo waliofanya makosa na kutafsiri kilio cha Pinda mbele ya Bunge kama njia ya kutubu. Hii ni baada ya Pinda kutoa kauli ‘iliyopinda’ ya kuchochea watu wajichukulie sheria mikononi kwa kuwaua watuhumiwa wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi - albino.

Je, kiakili hii inatosha? Je, Pinda kweli aliwalilia wahanga au alilia kuepuka hatari ya kukumbwa na yaliyomkumba mtangulizi wake, Edward Lowassa, baada ya kutajwa kuwa alishiriki ufisadi?

Tuzidi kufikiri. Je, kama Pinda kweli alikuwa na uchungu wa kuwalilia wahanga wa uzembe wa serikali, alishindwa nini kuiamuru serikali yake ichukue hatua za kisayansi na za kiusalama badala ya kukalia majanga ukiachia mbali kuwa majanga ni sehemu ya maisha ya Watanzania?

Nadhani baada ya Pinda kugundua kuwa Watanzania wameamka na walikwishaonya hili kwa kuwatimulia mbali vigogo waliokumbwa na kashfa, aliamua kucheza karata ya kutaka kuonewa huruma. Hii ni janja si kutubu. Tusidanganywe nayo. Tufikiri zaidi.

Kama Pinda kweli ana uchungu na wahanga, tuseme Watanzania, kwanini anakubali kuwa sehemu ya serikali iliyoshindwa na kuwaangusha Watanzania ukiachia mbali kuwasaliti na kuwatoa kafara kwa wawekezaji huku ikiwakingia kifua mafisadi? Rejea tamko la rais Jakaya Kikwete kutaka tumuache mtangulizi anayekabiliwa na tuhuma za kuiba mali ya umma.

Je, Pinda hajui kuwa uzembe wa serikali, hasa kwenye kushughulikia ufisadi, ndiyo chimbuko na kichocheo cha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, vikongwe na vibaka?

Hakuna siri. Pinda sawa na wewe, anajua jinsi watu wanavyoabudia utajiri upatikanao kwa njia haramu kama ufisadi, rushwa, mihadarati na mengine mengi. Wanafanya hivyo baada ya kuona wahalifu wakivumiliwa, kulindwa na kuheshimiwa.

Mtu yeyote aliyepata utajiri kwa kuwaibia Watanzania au kuwatoza rushwa, hana tofauti na auaye watu wenye ulemavu au vikongwe. Kifo ni kifo. Hakuna kifo kizuri wala chenye afadhali.

Kama tutafanya ‘homework’ yetu vizuri, tutagundua kuwa kashfa ya Pinda ni ushahidi wa kushindwa kwa serikali. Na serikali inayoshindwa kulinda watu wake na mali zao haipaswi kuendelea kuwa madarakani. Hapa ndipo umuhimu na ulazima wa kumng’ang’ania Pinda ajiuzulu tena mara moja unapoonekana.

Hatuwezi kumsamehe Pinda kwa sababu hatujui amri yake ya kutaka watakaokamatwa kwa kushikiwa kuwaua watu wenye ulemavu wa ngozi wauawe itaua wangapi. Tusijidanganye na kulia kwa Pinda.

Athari ya maagizo yake itakuwa kubwa huko tuendako. Kwanza ifahamike kuwa si watanzania wote, hasa wale wa vijijini aliowashauri waue huko mikoani wamesikia na kuelewa kitubio chake.

Kinachokera zaidi ni ile hali ya kitubio cha Pinda kulazimishwa na wapinzani badala ya bosi wake yaani Rais Kikwete! Ni ajabu kwa Kikwete kuchelewa hata kukaa kimya huku akiwaaminisha Watanzania kuwa ana sera za kuleta maisha bora kwa kila mtanzania wakati ukweli ni kinyume. Ukitaka kuliona hili, tathmini serikali ya Kikwete ambayo imekuwa madarakani kwa miaka mitatu sasa. Je, imetimiza ahadi gani zaidi ya kukumbwa na kashfa kila uchao?

Je, kwa hali ilivyo, kuna matumaini na mikakati ya kutimizwa kwa ahadi hata moja? Iwapo kipindi cha kuwa madarakani kimeshakatika kwa zaidi ya 3/5 na hakuna lililofanyika, Kikwete na wenzake watatenda miujiza gani kutimiza ahadi na matarajio ya umma?

Ajabu, ukiangalia vizuri, anachofanya Kikwete ni kuanza harakati za kuwania urais 2010 huku akiwa hajatimiza ahadi hata moja! Ameshindwa kutimiza ahadi. Hata kuwa na serikali adilifu ameshindwa? Rejea kwa mfano kuendelea kujizungushia watu wachafu chamani na serikalini.

Chukulia mfano kitendo cha hatari na kutia mashaka cha mkewe, Salma Kikwete, kuendelea kukusanya fedha zisizo na uhakiki kihesabu chini ya NGO yake ya Wama. Kwa nini kuwe na Wama iwapo wakati kuna wizara ya wanawake na watoto? Ajabu! hawa ndiyo wanaotuaminisha wataleta mabadiliko wakati ni wagumu kubadilika!

Kwa nini Kikwete hakujifunza kwa yaliyomkuta mtangulizi wake, mzee Mkapa, ambaye amejikuta matatani kutokana na tamaa za watu waliokuwa wakimzunguka?

Turejee kwa Pinda. Kwanza ikubalike. Maisha ya binadamu hata kama ni kichanga yana thamani kuliko kitu chochote, hivyo kitubio cha Pinda hakiwezi kulinganishwa na maisha ya makumi yatakayouawa au ambayo yameishauawa.

Asituhadae kwa kudai ana uchungu na wahanga. Hana uchungu. Angekuwa nao, tena kama mwanasheria na kiongozi wa ngazi za juu, angewahamasisha wananchi kujilinda kwa kufuata misingi ya sheria. Angewafundisha umuhimu wa haki za binadamu ambayo kila mmoja anapaswa kuifaidi wakiwamo wahanga.

Je, ni kwa nini Watanzania wanaonekana kufanya makosa kumsamehe Pinda? Inawezekana hawajui kuwa kimsingi wanayepaswa kumuandama si Pinda peke yake bali serikali nzima isiyowahakikisha usalama.

Pinda, sasa anaonekana shujaa kwa serikali kutokana na kuiokoa na hasira za Watanzania. Hana tofauti na Lowassa ambaye kuachia ngazi kwake haraka kulilenga kukinusuru chama chake kama ilivyokuja kujulikana baadaye. Na ndiyo maana akaendelea kulipwa malipo ya kustaafu wakati ukweli ni kwamba alifukuzwa.

Watanzania kama wanataka kujikomboa, wanapaswa kutumia fursa hii kuibana serikali itimke. Tuna hali tete kama ya Zimbabwe. Bahati mbaya upinzani wetu nao ni wa hovyo, unangoja kushindana kwenye uchaguzi utakaoandaliwa na kuendeshwa kwa wizi na mizengwe kama ambavyo imegeuka kuwa kawaida.

Hivi Kenya na Zimbabwe wangengojea uchaguzi wangefika popote? Serikali inaposhindwa kutawala kama ilivyobainika kwenye kashfa ya mauaji ya Pinda, hutimuliwa. Tutaendelea kutoa misamaha mingapi?

Tunapoandika kuna ushahidi wa wazi kuwa asasi na makampuni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vilishiriki kuliibia na kulihujumu taifa kwenye kashfa ya EPA na Richmond, lakini ajabu Watanzania wameendelea kuwaamini walioasisi wizi huu ili kupata hongo ya kuingilia madarakani watende haki?

Leo tuna mawaziri wa zamani kama Andrew Chenge, ambaye ushahidi unaonyesha wazi alishiriki kwenye ufisadi katika manunuzi haramu ya rada na ndege ya rais. Wapo kina Basil Mramba na wengine wengi. Wamefanywa nini licha ya Uingereza kutoa ushahidi wote hadharani?

Tunao mwanasheria mkuu wa serikali, Johnson Mwanyika, na mkurugenzi wa asasi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU) ambao waliguswa moja kwa moja kwenye uchunguzi wa kashfa ya Richmond. Ajabu watuhumiwa hawa bado wanakaa kwenye ofisi zetu kwa ridhaa ya rais utadhani ofisi zetu ni mali binafsi ya rais!

Tubadilike na kuweka hatima yetu mikononi mwetu badala ya kutegemea watuhumiwa wajishitaki. Na hii ndiyo sababu ya wezi wa Kagoda kutokamatwa maana wanaoambiwa wawakamate Kagoda ni Kagoda wale wale wa nyuma ya pazia.

Tumalizie na Pinda kama tulivyoanza naye. Kinachopaswa kufanyika kuhusiana na kashfa ya Pinda, kwanza ni kuiita kashfa badala ya kumlazimisha atubu. Kutubu si jibu.

Pili tuikabili serikali kwa ushahidi wa maneno ya Pinda na kutamalaki kwa rushwa na ufisadi ikae kando wenye uwezo wa kutuongoza wafanye hivyo. Kulia lia hakutusaidii kitu bali kutuongezea machungu. Nao ni usanii.
Chanzo: Tanzania Daima Februari 17, 2009.

3 comments:

Anonymous said...

Hello everybody, I just registered on this lovely forum and desired to say hello there! Have a extraordinary day!

Anonymous said...

Just popping in to say nice site.

Anonymous said...

Hi all! I'm from London but am living in Berlin at the moment.
Gotta like this place!


____________________________________
[url=http://stephetteh.wordpress.com/]Barrater is my life[/url]