The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Sunday, 3 August 2025

Kila Mwanandoa ni Mwanafunzi na Mwalimu

Wahenga wanatuasa kuwa elimu ni ufunguo na pia, katika kuisaka, hakuna mwisho. Elimu, kama hewa, iko mahali pote na popote. Inaweza kutoka au kutolewa na au kwa yeyote ilimradi mhusika awe tayari kujifunza na kufundisha. Hivyo, wanandoa, nao, kama waja, wana jukumu la kujifuza. Katika maisha, kuna vitu vidogo lakini vyenye thamani ambavyo hatuvijui tupaswavyo kufundishwa au kufundisha.
            Vitu hivi vidogo, vinaweza kusababisha makubwa yawe mabaya au mazuri. Mwanandoa awe tayari kujifunza na kufundisha. Hivyo, kuwa kabla ya kuwa mwalimu lazima uanze kuwa mwanafunzi. Na mwalimu wako si lazima awe na shahada au kusomea ualimu. Yeyote anaweza kukufundisha, na baadaye nawe ukamfundisha. Haya ndiyo maisha. Ni nipe nikupe.
            Katika kujifunza na kufundisha, tofauti na shuleni, wanandoa hawapati wala kutiana adabu wala kutoa adhabu. Hawapeani alama za ushindi au kushindwa. Kinachozingatiwa ni faida za kujifunza na kufundisha ili kuwepo amani, ufanisi, na upendo vya kweli baina ya wawili. Kujifunza hata kufundisha haviepukiki kwa wanandoa hasa ikizingatiwa kuwa, wanapopata watoto, hugeuka uwili yaani waalimu na wazazi. Je, kama hawako tayari kufundishana na kujifunza, wanawezaje kuwafundisha watoto wao? Pia, katika kujifunza na kufundisha, kunahitajika uvumilivu wa hali ya juu hasa ikizingatiwa kuwa wanadoa siyo watoto wadogo wanaoweza kutishwa au kuogopa kuadhibiwa.
            Mfano mwingine toka kwenye ndoa yetu ni tabia Nkwazi ya kudhani kila mtu alikuwa akijua na kuelewa kama yeye. Kabla ya kuoa, Nkwazi alikuwa na uthubutu hata wa kumwambia mtu aliyekuja kumtembelea aondoke kwa vile alilkuwa amechoka na kutaka kupumzika. Tabia hii ilimchukiza Nesaa. Aliamua kuikabili na kusema wazi kuwa ilikuwa mbaya. Taratibu, tuliua tabia hii yenye kuwaumiza wengine hata kama ilikuwa inaweka huru. Tuligundua kuwa maisha ni kubebeana mizigo na kutoa na kupokea baadhi ya haki. Hivyo, ghafla, yalitokea mabadiliko tokana na msukumo wa Nesaa.
            Kuna mifano mingi. Binadamu, siku zote, ni mwanafunzi, ndiyo maana wahenga walisema elimu haina mwisho na haipatikani darasani tu. Maana, dunia ni darasa tosha na maisha ni mwalimu tosha. Kama tuko radhi kujifunza toka kwa wanyama, majira, ndugu na marafiki, tunashindwa nini kujifunza toka kwa wenzi wetu?
Wengine wanaweza kukudanganya au kukupoteza au kutokupa uzito. Lakini mwenzi wako si rahisi kukupoteza au kukupuuzia kama kweli anajua thamani ya ndoa. Maana, kila upatacho ni chenu wote. Ni kwa faida yenu. Na isitoshe, ukiharibikiwa, naye anaharibikiwa, kadhalika ukifanikiwa, wote mnafanikiwa.
            Je, katika maisha ya kisasa ya tamaa na haraka, nani anakaa kumchunguza mwenzie na kumueleza anavyomuona katika tabia na hulka? Pigilia mstari hapo hujachelewa. Msome mwenzio na mueleze unavyomchukulia. Hii ilinitumbusha wanandoa fulani ambapo mmoja alipata ugonjwa wa meno na jino moja kuoza. Mwenye kuoza jino lililokuwa likitoa harufu, alipenda sana kubusiwa. Mwenzie alivumilia yote, na hatimaye akamshauri wakang’oe jino na kero ikaishia hapo hapo!
            Je, ni wangapi wanajikuta katika hali hizi wanaishia kupeana migongo badala ya kulikabili na kulieleza tatizo na kulitatua? Jambo la kushangaza ni kwamba aliyekuwa anaugua jino hakuwa akijua adha aliyokuwa akiipata mwenzie zaidi ya kulalamika maumivu tu! Ukiona mwenzio ana tatizo au udhaifu mkabili na msaidiane kutafuta jibu. Naye mwenzio anapoelezwa asichukulie kama anavunjiwa heshima. Ni nani anaweza kujichukia kwa sababu amegundua ana kidonda mwilini mwake?
            Sisi tulijijengea utaratibu wa kuandikiana barua za kesi wakati wa kutokuelewana. Anayehisi amekosa au amekosewa humwandikia barua mwenzie na kuiweka ima kitandani au sehemu tuliyokubaliana na kutoka ili mwenzie apate kuisoma na hatimaye ama kujibu au kuanzisha mjdala juu ya tatizo na chanzo cha kutokuelewana. Kumbuka tunaofanya hivyo hatuishi vyumba tofauti. Tunaisha chumba kimoja na kulala kitanda kimoja lakini bado tunaandikiana barua. Njia hii imeonyesha maajabu. Maana, kila mtu anapokuwa anaandika huwa yuko huru na pekee. Hivyo uwezo wake wa kufikiria unakuwa mkubwa ukilinganishwa na wa yule anayejitetea mbele ya mtu mwenye hasira anayeongeza maneno au hasira. Ijaribu uone.
Chanzo: Mwananchi leo.

Fyatu amkumbuka Ben Nkapa (RIP)

Japo wengi hawajui, Ben Bill Nkapa alikuwa fyatu wa kupigiwa mfano tena personal friend wa Fyatu mwenyewe. Nakumbuka emails zake za mwisho alizoniandikia. Naona yule anatikisa kichwa kuwa nazua au kutaka kuwafyatua wasomaji wangu. Usifanye hivyo. Fyatu Ben alikuwa rafiki yangu taka usitake. Kimsingi, niliunganishwa naye na Fyatu mwingine ambaye pia ni rafiki yangu Dingi wangu Pio Nsekwa. Hayo tuyaache. Yanatosha.
        Leo, kwa huzuni na majonzi, naandika waraka huu kumkumbuka Fyatu Ben. Kama raia wake na rafiki, nina jukukumu la kumkumbuka gwiji huyu aliyetoweka miaka mitano iliyopita. Wengi wanamkumbuka kwa ufyatu wake hasa kujiamini na kutoa hotuba ndefu tena zenye mashiko na zenye kujaa mapwenti. Wapo waliomuona kama mtu asiyefikika. Ukweli ni kwamba Ben alikuwa muungwana na down to earth sina mfano. Kwa wasiomjua, alikuwa tofauti na ninavyomueleza kama Fyatu aliyemfahamu.
        Kwanza, nikupe habari mbaya. Yule dogo aliyekuwa akikuhusudu  yaani rais Joni Kanywaji Malock si alikufa ghafla mwaka mmoja baada yako. Huu msiba ulitikisa taifa na dunia usipime. Wengi hadi leo hawajaamini kuwa gwiji huyu aliyesifika kwa kujiamini na uchapakazi alirejesha namba. Hata hivyo, aliacha alama ambazo zitachukua mamia ya miaka kusahaulika. Alianzisha miradi lukuki na kuipaisha kaya usipime. Baada ya kuondoka, makamu wake Bi Mkubwa Samia Solution alichukua ukanda. Maza anajitahidi usipime. Baada ya kushika ukanda, hajakaa hata kidogo. Anachapa kazi usipime. Baada ya Hapa Kazi Tu, alikuja na Kazi Iendelee. Na kweli, kazi inaendelea kindakindaki. Ukiachia politics za kukomoana na kupakaziana za wale wanaomuone maya na vivu, kaya imetulia. Ina amani na mshikamano na Bi Mkubwa wetu anazidi kuipaisha kaya. Mfano, lile daraja la Busisi ambalo sasa linaitwa JPM, lishakamilika zamani gani. Ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nchonga nao, si haba, uko karibia ukingoni. Unakumbuka chimbuachimbua ya SGR? Basi, mwanangu, inazidi kupaa ikielekea Burundi na Rwanda. Miradi ni mingi aliyokamilisha Bi Mkubwa. Nakumegea hiyo kiduchu tu.
        Mpendwa Ben, sasa tunaingia kwenye uchakachuaji, sorry, uchaguzi mkuu ujao. Chama twawala kishaandaa visu kupeta hata kama ni kwa bao la nkono kama alivyowahi kuseme Nipe Mapepe Ninaye kabla ya kuonyeshwa mlango. Kilishapata mpeperusha bendera yake ambaye ni Maza mwenyewe japo wapo wanaokosoa namna alivyopitishwa. Mambo ya Ngoswe tunamwaachia Ngoswe mwenyewe. Kama ujuavyo mambo ya mapinduzi mapinduzi hasa ya kifyatufyatu, kuna kitimtim cha kufa fyatu. Mafyatu sasa si haba. Wanajinoma kwa takrima na ukarimu vya muda wakijua wazi kuwa watafyatua njuluku za wanene sasa ili baadaye nao wafyatuliwe kwa miaka mitano ijayo.
        Juzi si kiliumana. Walitokea wachumia tumbo na matapeli tena toka kwenye chama twawala wakataka kukinukisha. Mmoja ni yule jamaa wa kujipachika mavyeo makubwa ya utukufu kama uaskopo, udoktari, mengine mengi tena akipiga njulukub kwa kuwaibia mafyatu walioishiwa eti atawafanyia miujiza waukate wasijue utawakata.Si jama alikinukisha akijifanya eti kupinga utekaji na upoteaji wa mafyatu! Wanaomjua walimshangaa kwa namna alivyotaka kuwadanganya mafyatu akiwamo yeye mweyewe. Jamaa alilituhumu lisrikal na chama harafu akajifanya eti yeye ni mwanchama kindakindaki wakati ni msaka ngawira na twapeli wa kawaida. Jamaa alishukiwa usipime. Lile duka lake la kuuzia neno na roho si lilifungwa kiasi cha jamaa kutokomea na kuishia kubwekea kwenye mitandao. Mpaka ninapoandika, jamaa hatouonja tena uishiwa ambao nao alikuwa amepewa na mwendaze.
          Mwingine ni yule jamaa mhuni mhuni aliyeibuliwa na mwendazake anayewaita wenzake wahuni kana kwamba yeye siyo. Huyu naye amekuja na mpya. Anapakaza eti hakuna haki kayani! Mafyatu tunajiuliza. Je, hii haki imeanza kutoweka hadi kutokuwepo lini na alikuwa wapi mbona hakuzoza? Kwa wanaokumbuka mwendaze alivyofumua kila kitu kiasi cha mafyatu kuanza kutoweka na kutoweshwa huku wengine wakimwagiwa shaba, anashangaa huyu jamaa alikuwa wapi. Fyatu sishangai. Si yeye ndo alikuwa jikoni mwa mwendazake akifyatua misimamo ya kuunga mkono kila kitu.
        Mpendwa Ben, rafiki yako na mshirika wako Anna bado anadunda ingawa miaka ndiyo hiyo inayoyoma. Bado anamudu mikiki ya maisha kama wengine. Ila haonekani sana kama zamani. Cha mno, tunakumiss we acha tu. Tunamiss falsafa yako ya uwazi na ukweli ambao wakati mwingine, wasiokujua uzuri wala falsafa yako walidhani ulikuwa ufichi na otherwise.
        Kwa vile uko kwenye pumziko la milele, naomba nisikuchoshe na mambo ya politiki. Japo, kwa ufupi, nimekupasha machache kati ya mengi yanayojiri huku uzimani. Naomba uwasalimie magwiji na mashujaa wetu walioko huko. Waambie tunawaenzi na kuwamiss sana kifyatu na kinomi. Unasalimiwa na best wako Pio Nsekwa. Siku hizi ameacha kuandika japo siyo kusoma. Huwa tunasalimiana mara kwa mara na kukukumbuka.RIP Ben Bill Nkapa my best friend.
Chanzo: Mwananchi Jtano iliyopita.

Wednesday, 23 July 2025

Fyatu kufyatua na kujinoma na king’ora!


Baada ya kuchoka msongamano wa Bongo isiyo na bongo za kutatua changamoto na kero zake, nimechemsha bongo. Niwajuze waziwazi. Nina mpango wa kununua na kufunga king’ora kwenye mchuma wangu kuepuka kusota kwenye foleni kama mafyatu makapuku wakati mie ni munene wao kama wale wanene wa kaya. Maana, kama sikosei, ndiyo mfumo wa kifyatu wa wanene kuwafyatua wachovu waliofyata badala ya kufyatuka na kufyaua wale wanaowafyatua tena kifalafala kama hivi. Kifyatu, hii inaitwa sera ya kujipendelea au kujihudumia ukijidai unawahudumia. Unawahujumu badala ya kuwahudumia kwa vile hawawezi kujihudumia kwa kukufyatua.  
            Unaweka ving’ora kwenye ndinga za wanene hata wale uchwara hukwepa madhara kiasi cha kutotafuta suluhu ya tatizo la msongamano. Zamani, wanene wakila baada ya wanyonge kula. Siku hizi, ni tofauti. Wanene wanafyatua kila kitu wakati wote tena bila aibu. Hakuna cha wanyonge wala wanyongwaji. Hizi zama za wanyongaji kuwanyonga wanyongwaji. Na hii, kinene, inaitwa haki ambayo hutokana na amani, utulivu, na “mshikamano” hata kama ni vya imani. Huoni kinavyoshikana barabarani siku hizi?
        Kwa vile hakuna kisichowezekana kwa mafyatu, wakiamua, nami lazima nifyatue king’ora kuepuka msongamano usababishwao na ukosefu wa ubunifu na uzwazwa wa kimfumo na kijamii.
        Kwanza, inakuwajekuwaje jamii nzima inaparaganyikiwa na kukosa mfumo uingiao akilini? Kwa vile mie mjanja tena mwenye akili kubwa ambaye nimeamua kuzitumia kuweka king’ora, hili swali si langu bali lako.
       Pili, kwa vile mimi ni munene wa mafyatu tena mjanja wa aina yake, na familia na washikaji wangu lazima waufaidi unene wangu. Hivyo, napanga kufyatua ving’ora kama sina akili nzuri. Nahakikisha, kama ndata na wanene wengine, bi Mkubwa wangu na kitegemezi chetu nao wanakuwa na ving’ora kwenye ndinga zao. Bila kufanya hivyo, bi Mkubwa anaweza kuwa anachelewa kila aendapo kusuka au kuchonga na mashoga zake huku kitegemezi kikichelewa shule. Sipati picha vitegemezi visivyo na ving’ora vinawezaje kuwahi shule na kusoma kama itakiwavyo mbali na kuamsha mapema na kuchelewa kurejea nyumbani.
        Tatu, licha ya kuweka ving’ora kwenye ndinga zetu, nataka kuanzisha utaratibu wa kufunga barabara ili misafara yetu ipite hata kama tunakwenda kupiga ulabu. Who cares kama mafyatu wameshindwa kufyatuka na kufyatua hadi wakafyata na kufyatuliwa kirahisi hivi unataka nifanye nini zaidi ya kuwafyatua kama wale wanaowafyatua nao wakafyata?
        Nne, rasmi, kuanzia sasa, nitahakikisha kila bodaboda itakayikaribia nilipo au kunipita, kufunga njia, au kujishebedua na kujifanya ina haraka, nachukua cha moto mkononi ili wakigonga ndinga yangu niwawahi kabla hawajaniwahi. Bila cha moto usawa huu, sijui nani atakuwa salama.
        Tano, kuanzia sasa, nataka kununua magwanda kama ya ndata ili ikitokea kikaumana au kunuka, mafyatu wajue mie ni ndata. Hivyo, wanigwaye hata kama nitagonga mikweche na ngwalangwala zao uchwara au siyo? Maana, usawa huu, bila kwenda kindavandava mambo hayaendi zaidi ya kuishia kufyatuliwa hivi hivi ukijiona kama kaya ilivyofyatuliwa hadi wenye akili kuhoji utimamu wa akili zetu.
         Sita, baada ya kufunga king’ora, sitapita kwenye barabara za kawaida zilizojaa mikweche na misongamano. Yangu ni Mwendo Kasi tena kwa kasi na visasi kama wenye ving’ora na bodaboda wafanyavyo bila kustukiwa wala kupewa adhabu japo ya faini. Unacheza na kaya hii isiyo na mpangilio wala mfumo vinavyoelekea zaidi ya vurugu? Kila fyatu anatungia na kujichagulia sheria yake.
        Taa ikizuia, bodaboda anakula mwendo. Ikiruhusu kwenda kulia, yeye anakwenda kushoto tena na ndata wanaangalia. Sijui wapo pale kama au maua au mapambo au kuna jambo? Mbona nasikia kwa Ka-game wanafuata sheria kama madereva wengine? Kwani, hapa tatizo ni bodaboda au wanene walioruhusu hii vurugu. Au nishauri mafyatu watumie bodaboda tuone itakuwaje. Kama mbwai mbwai du. Ama kweli kaya imefunguka kiasi cha barabara kufungwa kwa mafanikio. Hapa lazima tuseme wazi. Bodaboda mnaupiga mwingi.
        Saba, kwa vile mimi ni munene na nina mtandao mkali, napanga kupeleka kitegemezi chetu kusome majuu kuepuka kuzeekea kwenye ngwalangwala kikienda shule ambako bila shaka kitafeli tu. Unacheza na foleni na vurugu siyo?  
         Nane, napanga kuitisha bunge la mafyatu ili kutunga sheria mpya ambayo itaitwa uhasama na vurugu barabarani badala ya ile ya usalama barabarani ambayo imegeuka fujo barabarani. Hapa, nitapendekeza taa na vitochi na matrafiki wote waondolewe barabarani ili kupunguza fujo na vurugu. Nitashauri hata mataa ya barabarani yaondolewe na kuweka tunguli. Maana, Waswahili wanavyoogopa tunguli, bila shaka, watazitii kinyume na wanavyodharau mambo ya sayansi na tekelinalokujia.
        Mwisho, kwa vile ving’ora vinalipa na kuepusha usumbufu na vurugu, napendekeza wanjanja wote tuwe navyo ili kuepuka kunyotolewa roho na misongamano na misongo ya mawazo vitokanavyo na uholela huu na uzwazwa vya kujitakia. Ving’ora hoyeee! Du! Kumbe naota mchana!    
Chanzo: Mwananchi leo.

Tuesday, 22 July 2025

Wanandoa msijidhalilishe hata uwe na shida vipi

Kuna kisa kimoja kilitokea huko Mombasa Kenya. Bwana mmoja alikuwa na mkewe pamoja na watoto. Huyu bwana alikuwa akitafuta riziki zake kwa kuongoza watalii kwenye pwani ya Mombasa. Siku moja, alimpata mzungu mwanaume aliyetokea kuzoeana naye. Huyu mzungu, kila akija, humwambia amtafutie wanawake wa kufanya nao ngono kwa malipo aliyoona manono kwake.
            Mara ya kwanza, huyu bwana alimtafutia mteja wake wanawake na kumalizana naye. Kwa vile ni watu waliokuwa wanaishi eneo moja, yule mteja alikwenda kumshukuru yule baba kwa kumtafutia mteja aliyemlipa vizuri. Hivyo, alimkatia pesa nzuri sana tokana na ukuwadi wake. Yule baba alishangaa kugundua kuwa kumbe yule mteja wake alikuwa akiwalipa pesa nono wanawake aliokuwa akiwachukua.
             Mara ya pili, yule mzungu alirejea baada ya miaka kama miwili hivi na akamtaka, kama kawaida yake amtafutie mwanamke wa kutumia naye kwa wakati ule ambao alikaa Mombasa. Hivyo, kwa kujua namna yule bwana anavyotoa dau kubwa, aliona kwanini riziki kwenda mbali wakati mkewe angeweza kutumika na kuingiza hicho kipato kinono?
                Kwa tamaa ya kupata asijue anaweza kupatikana na kujuta, alimshauri mkewe akubali. Kwenda kutumia naye na akakubali lakini akiwa anashangaa mantiki gani ya muwe kufanya hivyo.  Mwanzoni, alidhani mumewe alikuwa anamtega kuona kama alikuwa muaminifu. Hata hivyo, alipotaka mumewe amhakikishie kuwa si mtego, yule mama alikubaliana na mumewe kwa shingo upande asiamini kuwa mumewe hakuwa akimthamini kiasi hicho kiasi cha kumgeuza kifaa cha kutafutia riziki. 
            Pamoja na kukubali ushauri wa mumewe, mke aliona kama anadhalilishwa na kuamua kuondoka na yule mzungu. Hivyo, pamoja na kukubali kwenda, alipanga namna ya kumkomesha mumewe aliyemuona kama alikuwa akimchukulia kama kifaa kisicho na thamani ya pekee kiasi cha kumkodisha kama gari au nyumba tena kwa malipo ya fedha. Kwa kujua thamani yake, yule mama, hakuona uzuri wa kwenda kufanya umalaya ili kupata fedha tena kwa kushauriwa na mumewe. Hivyo, aliamua ima aachane na yule mume au amridhishe yule mzungu lau ampe mtaji aanze maisha yake aondokane na aibu na utumwa huu.
          Kweli, kila aombaye hupewa. Yule mzungu alitokea kumpenda yule mama kiasi cha kutamani amuoe kama angekuwa tayari. Na bahati mbaya, yule bwana hakumwambia kuwa yule mama alikuwa mkewe. Hivyo, baada ya kunogewa na kuridhika, yule mzungu alimuuliza yule mama kama alikuwa ameolewa au kwenye uhusiano. Mama alimwambia kuwa alifiwa na mumewe miezi michache iliyopita na aliamua kumkubalia kutumia naye kwa sababu yule bwana aliyemtafuta alisema alikuwa ni mtu muaminifu sana. Mzungu kusikia hivyo, alizidi kupenda. Alimuomba amuoe lau aweze kuachana na mateso yaliyosababishwa na kifo cha mumewe.
                Kwa kujua, kuwa yule bwana angeweza kutibua dili, alimuomba waondoke kwenda kutumia Zanzibar, na huko wapange namna ya kwenda kufunga ndoa Ulaya. Mambo yalipangwa yakapangika. Wawili walienda zao Zanzibar kustarehe na baadaye kuelekea Ulaya tayari kuwa mke na mume. Kwa kuhofia mumewe angeweza kutibua dili, alimuomba waondoke kimya kimya kwa sababu yule bwana, yaani mumewe, aliyemkuwadia yule mzungu alikuwa akitaka wagawane fedha nusu kwa nusu kwa kuwa bila yeye asingepata mteja. Mzungu kusikia vile alichukia na kumuona mume wa yule mama hakuwa muaminifu na alikuwa mwenye tamaa kwa vile alikuwa akimlipa fedha ya kutosha kumkuwadia. Hivyo, alikubaliana na pendekezo hili kirahisi.
                Yule Bwana alishangaa maana, alitegemea mkewe angerejea asubuhi. Alipoona harejei, alijiaminisha kuwa alikuwa amepewa dau kubwa la kutumika kwa zaidi ya siku moja. Hivyo, hakuwa na shaka mkewe angerejea na kibunda cha kutosha asijue hatamuona tena maisha yake yote.
            Vitu hata viwe na thamani gani, unaweza kuuza, kukodisha hata kugawa lakini si mtu. Je hapa tunajifunza nini? Ungekuwa wewe ungefanyaje? Je uamuzi wa yule mama kuondoka maisha yote ilikuwa ni uamuzi mzuri au mbaya?
            Somo kubwa ni kwamba mwenzi wako ana thamani kuliko kitu chochote. Hivyo, hata uwe na shida au changamoto kiasi gani, achia mbali kumtumia kama kitu. Hata kufikiria ni dhambi isiyo na msamaha. 
Chanzo: Mwananchi Jpili iliyopita.

Wednesday, 16 July 2025

Kwanini tusiite kaya Chaitan au Tanghasia?

 
Juzi, katika kupitapita mitaani kutoa tongotongo, si nikachekwa kiasi cha kudhani naanza kuchizika. Kwanza, kituko kilianzia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bole pale Addis. Baada ya kutua kama kawa, hutoa tongotongo. Hivyo, nilikwenda kwenye ofisi za shirika la njiwa la Ethiopia lenye watumishi wa hovyo sina mfano. Mstuko ndo usipime. Nikiwa nimejipanga mstarini tayari kusikilizwa, niliomba msaada kwa abiria mwengine aliyekuwa mbele yangu ambaye ni mmakonde kama mimi. Ukiachia yeye na wengine wachache, abiria tarajiwa wa njiwa hiyo waliobakia walikuwa wachainizi!
                Nilimuuliza jamaa kama kuna njiwa mbili moja ya kuja Ufyatuni na nyingine ya kwenda Chaina. Jamaa alishangaa. badala ya kujibu swali, naye aliniuliza swali. Si unajua tena mafyatu. Badala ya fyatu kujibu swali langu, naye aliswalika swali. Alisema “kwani wewe unelekea wapi?” Nilimjibu kuwa nilikuwa natia timu kaya. Badala ya kunipa jibu aliuliza tena “kwani tatizo lako nini? Baada ya kuona hivyo, nikanywea na kuamua kujiondokea nikangoja wakati ukifika wa njiwa wangu kupaa nitangoja mtangazaji anijuze ni ipi.
            Baada ya kusota muda mrefu na muda wa kupaa kuwadia, nilienda tena kwenye geti la kupandia. Kwa mara nyingine, nilikuta wachaina kibao. Hivyo, ilibidi nimuulize mfanyakazi mmojawapo kama njiwa iliyokuwa inaondoka ilikuwa inaelekea Chaina au Ufyatuni. Akiwa ameshangaa kidogo, alijibu kuwa ilikuwa inaelekea Ufyatuni na si Chaina. Du! Nilianza kuskuti lau nipate jibu nisipate. Basi, Fyatu nilifyata nikingoja pipa litue nione yaliyokuwa yakinisibu kuhusiana na hawa wachaina. Kutua, tu, nikasikia wengine wakitema uswa japo wakichainachaina.
            Nilichukua ndinga yangu kuzama zangu Utashani kwa wenzangu. We bwana! Kufika, si nikakuta hata apartments za kupangisha baadhi yake zinamilkiwa na wachaina. Kabla mstuko kuniisha si nikasikia mmoja akipita akisema ‘nauja ice cream!” “Du” nilijisemea “utadhani niko zangu Uchainani na si Ufyatuni!” Baada ya hapo, maswali lukuki yalianza kunishambulia. Hivi huu ndiyo uwekezaji au uchukuaji kama siyo exportation of jobless army from Chaina?” Nisameheni kwa kitasha. Maana, siku hizi hata Kiswahili naongea kwa taabu sana kiasi cha kuandika haya madude kwa msaada wa mshikaji wangu Siri. Hayo tuyaache. Kwa kuzingatia haya, kwanini Ufyatuni isiitwe Chaitan?
            Mbali na kuitwa Chaitan, maybe, chai tamu, lipo hili sekeseke na timbwili kama siyo mtiti wa haya jamaa zangu waendesha baiskili za umeme au Toyo. Da! Hawa jamaa walinikanganya hadi nikaongopa hata kuendesha ndinga yangu kwa wanavyoonyesha umahiri wa kuvunja na kuvuruga sheria za barabarani.
             Kwanza, nilijiuliza kifyatufyatu. Inakuwaje mafyatu wazima wenye akili timamu kama siyo kuchizika, na nguvu wafanye vitu ambavyo kwa kisambaa huitwa suicidal? Je ni kuchizika, ukosefu wa akili timamu (UAT), ukosefu wa ubunifu au kujichoka na kuchoka kuishi? 
            Pili, ni kwanini wahusika hawaoni denja wanayocheza nayo? Tatu, inakuwajekuwaje wanene hawaoni balaa hili ambalo naona ni kama bomu linalotika likingoja kuitafuna kaya? Nne, kwanini hawaoni uchafuzi wa mazingira mbali na uwezekano wa kutengeneza kizazi au taifa la viwete tokana na uvunjaji wa sheria na uendeshaji wa hovyo na hatarishi wa toyo unavyosababisha vifo vya waendeshaji na abiria? Tano, imekuwaje tumejichoka na kuruhusu ghasia kuwa ndiyo mfumo wetu wa maisha kama mafyatu?
            Kusema ukweli, sikuamini kuwa fyatu mwenye akili timamu ana anayetaka kuishi angeweza kupanda haya majeneza yasiyofunikwa yaitwayo toyo. Sikuamini kuwa kidude kinachopaswa kubeba mafyatu wawili tena wakiwa, kisheria, wanapaswa kuvaa helmet kwa usalama wao, kingeweza kupakizwa mafyatu watatu na wakati mwingine wanne. Funga kazi ni pale niliposhuhudia abiria wakipanda haya madude ya kifo bila kuvaa helmets. Je, hapa tatizo ni wahusika au mfumo mzima usiofuata maadili wala sheria bali madili na shari? Kwa mujibu wa hali na jinai, kwanini Ufyatuni isiitwe Tanghasia?
            Jambo la tatu ambalo ningepata nilidurusu japo kwa ufupi ni upigaji wa kizwazwa na wa kutisha, au tuseme wizi wa kimfumo. Mwajua kuwa juzi llikuwa Saba Saba? Siendi kwenye historia yake na kuzaliwa kwa chata la TANU. Katika kutoa tongotongo, si nikatinga nikiwa na lengo la kwenda kuwafaidi waanimo hasa lion. Kama kawa, nilificha njuluku na rukono yangu bila kusahau wallet yangu ili wale washenzi wasinisachi na kusepa. Kwa vile ni bonge la mjanja, njuluku niliweka sehemu nyeti na kusepa. Kufika tu, huo msongamano usipime. Katika kusukuti, si nilikuta kuwa ni wa kutengenezwa ili wahusika wapate kuuza hata tiketi feki na kusepa? Nani alilistukia hili? Hili halikunihangaisha kwa vile ulaji na madili ni sehemu ya mfumo wa Danganyika na Zaa inzi, we koma.
            Nilitaka kushambuliwa na presha pale nilipolipia tikiti ya kuingilia na kuishia kulipishwa tena kuwaona waanimo? Je huu siyo uanimo kunipiga kuwaona waanimo wakati nshalipia kuingia kuenjoy kila kitu? Kumbe nina jet lag inayochizisha akili?
Chanzo: Mwananchi leo.

Jengeni kwako siyo kwenu

Kuna baadhi ya wanandoa wenye tabia hatarishi, za hovyo na kinyonyaji kwa wenzao hata wao wenyewe. Hii yaweza kuwa jambo ambalo ni la kupanga au hata kutokea tokana na mazoea au ujinga wa aina fulani kama siyo ubinafsi na upofu. Kwa muktadha huu, si jambo geni kusikia kuwa mwanandoa, hasa akina mama, japo si wote, wakiwashinikiza waume zao kuwajengea wazazi wa wao nyumba, kusomesha ndugu zao, na mengine kama haya. Kwa lugha za mitaani hii ni ima chuma ulete au kuchuna buzi. Mambo haya yapo, na kuna baadhi ya makabila nyonyaji na wavivu wameyazoea kiasi cha kugeuza mabinti zao vitega uchumi.
            Utawasikia wazazi wakimuulizwa binti wao kazi au vyeo vya mtarajiwa wake. Wengine hujisifu kuwa mabinti zao wameolewa na watu matajiri au wakubwa kana kwamba wao nao ni wakubwa au matajiri. Hii ni aina fulani ua umaskini wa kijamii na kiuchumi ambapo utu wa mja huzidiwa thamani na vitu fedha na mali. Wengine huwambia kabisa kuwa wanataka binti awaletee mchumba wa aina fulani kana kwamba wao ndiyo wanaoolewa. Japo ni haki ya wazazi kutunzwa na watoto wao, wazazi wa aina hii ni vibaka au wezi wa kawaida wanaotumia mabinti zao kwa kuwageuza watumwa wa vitu bila kujali madhara yake.
        Kama wanandoa mna uwezo iwe wa kifedha au utashi, si jambo baya kuwajengea wazazi wa pande zote mbili kama hawakubahatika kujijengea. Pia, si vibaya kusomesha wadogo zenu na mengine kama hayo kama yatafanyika kwa faida ya pande zote. Hata hivyo, mfanye tokana na mapenzi na uwezo wenu na si mashinikizo toka kwa wazazi au wenzi wenu.  
            Muhimu, mnapofanya haya mambo ambayo yaweza kuwa majukumu yenu, msibague au kupendelea au kuutenga upande mmoja. Ajabu, hao wanaotaka wafanyiwe yote hayo, hawakuwafanyia wakwe zao! Hapo ndipo dhana ya jinai ya unyonyaji, uvivu, na wizi inapojengeka. Hata hivyo, hiki kinapaswa kuwa kipaumbele namba moja, yaani kuwajengea wao kabla ya kujijengea au kuwasomeshea watoto wao?
        Tuanzie hapa. Kwanza, tunajua. Wapo wazazi, hasa wenye uwezo, wanaowajengea watoto wao nyumba na kuwapa mali mbali mbali. Pia, wapo wanaowapa vyeo tokana na nafasi walizoshika. Hapa, tunaongelea wale ambao wana uwezo wa kawaida, yaani wanaoanza maisha. Je ni haki kuwajengea wazazi wenu hasa wa mke kabla ya kuwa na nyumba yenu wenyewe? Je, ni halali na sahihi kwa mmoja wenu kuweka kipaumbele upande mmoja huku akiuacha upande mwingine?
            Pili, kabla ya kutoa jibu au majibu, tuulize maswali tena. Kabla ya kuwajengea wazazi wenu, jiulizeni. Je wao waliwajengea mababu zenu? Kama jibu ni hapana, kwanini? Kama jibu ni ndiyo, je, walifanya hivyo kibaguzi na kwa shinikizo tena la upande mmoja? Kama kipaumbele cha mmoja wenu ni kuwajengea wazazi wake, jiulize. Kwako utajenga lini? Kwanini uanze na kwenu badala ya kwako? Je na mumeo akiamua kujenga kwao, nawe kwa wazazi wako, kwenu mtajenga lini? Je, kwako, ndoa ni kitega Uchumi au mfumo wa maisha tena ya kudumu baina ya watu wawili na jamii zao? Je hakuna namna ya kuwasaidia wazazi wenu bila ya kubaguana, kujiumiza, kuhujumiana, na kutumiana? Hivi, hali kama hii inapotokea, nani waathirika nan ani wanafaa kuwa wanufaika? Wakati mama ukimshinikiza mumeo awajengee nyumba wazazi wako au kuwasomesha wadogo zako, jiulize, hayo yangefanywa na wifi yako kwa wazazi wako ua mkamwana wako kwako, ungejisikiaje na kufanya nini? Hili ni suala na swali muhimu. Kulijibu uzuri, epuka dhana na imani ya mkuki kwa nguruwe. Wahanga wa jinai hii waweza kuonekana kama nguruwe wanaopaswa kupata mkuki bila kujua hawa wanaowachoma hii mikuki wanaweza kuwa nguruwe wa kesho.
            Hivi, inawezekana kuishi sehemu mbili au kutumia mabwana wawili kwa wakati mmoja? Je wanapoamua kuanzisha hujuma hii, huwa wahusika wanajiuliza kama wanaotaka kuwahujumu nao wana akili timamu hata kubwa kuliko zao? Jengeni kwenu kwanza kabla ya kwa wengine. Huu ni usia wa leo.
Chanzo: Jpili iliyopita.

Wednesday, 9 July 2025

Tumechanganywa, tumechanganyikana, na kuchanganyikiwa

Fyatu mwenzenu niliipata kinoma. Katika kupata ulabu si akatokea chawa mmoja akamshambulia rafiki yangu ambaye ni mchunaji, sorry mchungaji wa kujipachika. Ni wakati alipokuwa akisifia ufyatu wangu ninaotoa hapa. Fyatu sorry chawa alihamaki na kurusha matusi tena ya kitoto utadhani hakuwa fyatu mzima! Nilipohoji kunani, alisema tena kwa kebehi ‘inakuwaje huyu unamruhusu achanganye dini na siasa?” Nilimuuliza anachanganya dini na na siasa vipi au wewe ndiyo unavichanganya wakati vyote viwili ni dugu moja? Fyatu chawa alijibu “nimewasikia mkilaumu kila kitu anachofanya maza. Halafu mnasifiana.” Bila kupoteza muda, nilimjibu kuwa kazi yetu siyo kumsifia yeyote awe maza au faza yetu. Kwani, yeye ni malaika asiyekosea?
            Namshukuru huyu fyatu chawa maana, sikuwa na mpango wa kutumia wiki nzima nikifuatilia tulivyochanganywa, tukachanganyikiwa, kuchanganyana hadi kuchanganyika, kukachanganya uongo na ukweli vikachanganyikana kifyatufyatu. Hivi kuchanganya dini na siasa ni nini? Katiba wala sheria havisemi lolote! Je dini na siasa ni tofauti au watoto mapacha? Nitajibu swali hili mwenyewe, nawe uongezee. Kimsingi, taasisi hizi zina sifa zifuatazo:
            Mosi, Zote chimbuko lake ni ughaibuni kabla na wakati wa ukoloni. Umewahi kujiuliza kama kuna mchango wa wahanga kwenye kuanzishwa na kuingizwa vitu hivi ambayo hutumia maguvu yawe ya mitutu au imani? Sasa, jiulize, na ujijibu mwenyewe.
            Pili, vyote ni kolonishi, yaani, vinatawawala mafyatu na kuwatumia vitakavyo hata kuwachanganya kiasi cha kuchanganyikiwa na kuanza kuchukiana mbali na kunyonyana hata kunyotoana roho.
            Tatu, vyote hutegemea mafyatu kama mashamba yao na kuvuna visipopanda. Vikipanda, hupanda maneno na kuvuna njuluku. Mfano, siasa hutumia ushawishi hata ahadi za uongo kuwaingiza mkenge mafyatu ilhali dini hutumia vitisho vya moto na ahadi za vinono kuwatwisha mkenge mafyatu. Hamjaona pale Ubunguo? Fyatu mwenye duka lake la kuuza roho kasepa. Mafyatu wanafanya nini? Si wanakutana kila j’pili na kupigwa na ndata wakitetea fyatu asiyeweza kujitetea? Kwanini wasimuachie god wake amtetee? Si aliwahi kujidai kuwa hatishwi na yeyote wala chochote? Atokee na kufyanya fyoko akione cha moto.
            Nne vyote hutumia njuluku za mafyatu zwazwa bila kukaguliwa na yeyote kiasi cha kuwatajirisha matapeli wa kiroho na kuwasikinisha mafyatu zwazwa.
            Tano, vyote hudai vimetoka kwa God. Utawasikia hata matapeli wa kujipachika wakisema wao ni mashushu au wawakilishi wa god. Wanasiasa wakiukwaa ukuu, watakwambia maulaji yote hutoka kwa god. Hivi maulaji ya nduli au M7 yametoka kwa God? Mbona hamjui kitu rahisi hivi!
            Sita, vyote uahidi unono hata kama mwishowe ni uchungu. Kila siku, utasikia wanasiasa wakiahidi kuleta maendeleo yasiyofika! Ukichunguza ni maendeleo ya nani? Hili sijibu. Jibu mwenyewe.
Sita, vyote hufanya matanuzi na kukemea wafuasi wake kuyachukia. Utamsikia mwanasiasa fisadi akilaani ufisadi majukwaani wakati ni ufisadi huo huo mtaji wake. Tapeli wa kiroho atakwambia mbinguni wataingia maskini ilhali yeye ni mkwasi!
            Saba, vyote hupenda madaraka na ujiko. Kila palipo na kamera au waandishi wa umbea, lazima wawili hawa wawepo. Japo wanene wa dini hawakutangaza dini zao kama biashara, siku hizi, hata runinga na radio vinatumika kuwaingiza mkenge mafyatu.
Nane, vyote vilichanganyika tangu kuanza kwake kule Uropa ambapo popu alikuwa kiongozi wa lisrikal mbali na ntume naye kuwa mkuu wa dola. Kwani, hamjui au hamsomi historia?
Ngoja nichimbe zaidi. Dini na siasa vinachanganyikana na ni mapacha ila inategemea unavichanganyaje na kwa maslahi ya nani. Mfano, muimbaji wa nyimbo za injili akiimba nyimbo za kusifia wanene siyo kuchanganya dini na siasa. Akiimba za kukosoa, hapa, anachanganya dini na siasa kiasi cha kutishia amani na utulivu vya walaji na wanene.
            Siasa inachanganyikana na kila kitu.
            Mosi, mfano, mjeshi akiteuliwa kwenye nafasi ya kisiasa hachanganyi ugeshi na siasa?
            Pili, ndata akisimamia uchakachuaji au kupendelea chama twawala, hachanganyi undata na siasa? Nani anahoji au kukataza?
            Tatu, mchungaji wa bandia akijiunga na watawala, hachanganyi dini na siasa. Ila akikengeuka kutaka kuendelea kuwatumia, anaambiwa achanganya dini na siasa!
            Nne, waumini wakintetea bosi kwa sababu ni dini moja, wanachanganya siasa. Na lazima waonywe hata kufungiwa kwa kuleta udini na kuchanganya dini na siasa.
            Tano, wanasiasa wakiapishwa kwa vitabu vya dini, kuombe, ‘kubarikiwa’, kuchangia asasi za kidini, au kuhudhuria kusimikwa kwa viongozi wa kidini, hawachanganyi dini na siasa!
            Sita, waumini au viongozi wakilipa kodi wakahoji matumizi yake, wanachanganya dini na siasa!
            Saba, dini zikiwahimiza waumini kushiriki uchaguzi na kuchagua chama twawala, hawachanganyi dini na siasa.
                Mwisho, tunaposema dini na siasa havichanganyiki wakati tunavichanganya, huku si kufyatuka kuchanganyana na kuchanganyikiwa? Basi, tuchanganyeni tuchanganyikiwe tuchanganye na kuchanganyikiwa kama lengo ni kutenda haki na kuleta maendeleo vya kweli. Kifyatu, dini na siasa ni mapacha au nimechanganya kujichanganya, kuwachanganywa, kuchanganyana na kuchanganyikiwa?
Chanzo: Mwananchi leo.

Mafanikio yasikuvunjie ndoa

Kuna kisa cha mama mmoja aliyeukwaa uheshimiwa.  Tulipata kisa hiki kwenye pitapita zetu kwenye tarifa mitandaoni na kuthibitisha kuwa ilikuwa ni stori ya kweli. Tuliweza kudurusu na kujua hata jimbo analotoka katika mkoa mmoja wa Kanda ya Ziwa. Huyu mama, kwa kusaidiwa na mumewe, alitumia raslimali za familia kuukwaa uheshimiwa ambao, hata hivyo, uliishiwa kuwa uishiwa. Hii ni kutokana na kuvurunda na kuivunja ndoa yake baada ya ukubwa kumpanda kichwani.
            Pili, alianza kwenda ughaibuni akiandamana na waheshimiwa wenzake wa kiume na maafisa wakubwa wakubwa wa serikali. Huko, walikaa kwenye mahoteli ya bei mbaya wakila na kunywa na kulala pamoja. Ghafla, uzalendo ulimshinda. Alianza mahusiano yasiyo na heshima na waheshimiwa wenzake. Walipika na kupakua kiasi cha kunogewa. Jambo hili, lilimpelekea kutokuwa na hamu na mumewe kiasi cha kuanza kuanzisha kasheshe hadi ndoa ikavunjika.
            Tatu, badala ya mafanikio kufanikisha ndoa, yalifanikisha kitu kimoja tu ambacho ni kuivunja ndoa na kuacha majuto na mateso si kwake tu bali mume na watoto na hata ndugu na jamaa.
            Japo si wengi wala wote wanaojitokeza kueleza ukweli huu wa aibu na uchungu, je hawapo? Je ni akina mama wangapi wenye madaraka wamevunja ndoa zao? Je kwanini ni wanawake ambao ni wahanga wa madaraka au kuna na wanaume? Jibu laweza kuwa sababu ni kwamba jamii yetu inatawaliwa na mfumo dume ambapo wanaume wana uwezo wa kufanya watakalo na wasifanywe kitu na wenzi wao wa kike.
            Katika kudurusu kisa hiki, je nani wa kulaumiwa. Je ni mfumo au mhusika mwenyewe? Je hii inatoa somo gani kwa wale ambao hawajaingia na yakawakuta haya yaliyomkuta dada huyu ambaye wakati anaupata uheshimiwa alikuwa mdogo miaka 30 na ushei? Je hiki hakiwezi kuwa kikwazo kwa wanawake wengi ambao wangetaka kuingia siasa? Je wahusika wachague kipi kati ya madaraka na ndoa? Wakati mkitafakari kujibu maswali hayo hapo juu, tunaweza kuwapa mwangaza au ujanja wa kufanya uamuzi bora. Tutatoa angalizo kuwa madaraka ni ya muda na ndoa ni ya kudumu. Kwa mwenye akili safi na busara, atachagua cha kudumu na kuachana na cha muda. Je ni wangapi wanaweza kuchagua ndoa na kuachana na madaraka? Je hatuhitaji kubadili mfumo wetu wa kisiasa ili kulinda ndoa za waheshimiwa wetu na kuwahakikishia usalama akina mama ili wawe na mazingara salama na sawa kushiriki katika siasa? Je hili ni tatizo la watu binafsi au la jamii kwa ujumla pamoja na mfumo wake? Maswali ni mengi kuliko majibu.
            Pamoja na kwamba makala hii inahusika na ndoa za waheshimiwa na madhara wapatayo, inawakilisha dhana nzima ya madaraka kijinsia. Kwanini wanaume wanapopata madaraka hayavunji ndoa zao? Kwanini madaraka ni tishio kwa ndoa za akina mama wengi japo si wote? Je nini kifanyike?
            Je katika kudurusu kisa husika, wewe kama mwanandoa, unamsikitikia, kumlaumu, kumhukumu, au kutojali kwa vile hayakuhusu? Je ungekuwa wewe, ungechagua nini na kwanini? Tunauliza maswali hii kutaka kuwaelimisha wasomaji wetu kuwa madaraka si uheshimiwa tu bali ni dhana mtambuka. Kuna haja ya wanandoa kushirikiana katika jambo hata kama ni madaraka au mafanikio vinginevyo, yanaweza kugeuka maanguko si kwa mmoja bali wao, watoto wao, na hata wazazi, mafarafiki na familia zao.
            Tumalizie kwa kuwataka wahusika na jamii kwa ujumla kukomesha na kuepusha balaa hili kwa ndoa litokanalo na mfumo dume na fisasdi. Kwenye nchi za magharibi, waheshimiwa huchunguzwa sana na kupewa adhabu kali wanapopatikana kuvunja kanuni za maadili wanazopaswa kuzifuata. Hata hivyo, wana mazingira mazuri ya kuwezesha waheshimiwa kulinda. Nasi, baada ya kugundua tatizo hili, kama jamii yenye akili timamu, tuchukue hatua kulikomesha ili kuepusha mateso kwa familia nyingi na wanandoa mbali na kuwepo mazingira magumu kwa wanawake kufanya siasa kwa uhuru bila kuchelewa yaliyompata mhusika kwenye kisa husika.
            Baada ya kujaa mjengoni, kwanza, mama alianza kuzinyaka na kuuonja unono na utamu wa ukubwa. Mshahara alipata si haba tena kwa mamilioni. Milioni tano kwa mwezi mbali na marupurupu lukuki kiasi cha kuondoka na si chini ya milioni kumi kwa mwezi.
Chanzo: Mwananchi j[pili.

Thursday, 3 July 2025

Fyatu Kutoa Gari kwa kila Mpika Kura ya Kula

 

Kama mjuavyo, uchakachuaji, sorry, uchaguzi mkubwa umekaribia, na ninagombea urahis na lazima nitashinda hata kama ni kwa goli la mkono kama lile na Mapepe Tunaye. Hivyo, kwa vile mie ni muwazi, naweka wazi mikakati na ukarabati wa kushinda hii kitu mapema asubuhi kama ifuatavyo:

            Mosi, kuanzia sasa, nitamwaga ndinga kali na za bei mbaya za kisasa kuhakikisha kila mpika kura anapata moja ili anipe kura ya kula. Mie, siyo wa kumwaga vikwata wala tukutuku visivyo na utukufu zaidi ya utukutu. Si wa baiskili kama Sikiri maskini. Hivyo, kaeni mkao wa kula usawa huu wa kuvuna ambapo hamkupanda na kupanda ambapo hamtavuna.

            Pili, nimeamua kukopa njulu nje na ndani kuhakikisha mradi wangu wa ushindi unafanikiwa. Japo nimesikia baadhi ya mafyatu wakizoza na kupayuka kuwa nakopa sana, wanataka nifanye nini? Nani kawaamba kuwa kukopa ni kosa wakati ni harusi ingojeayo matanga ya kulipa kwa walipaji? Najali nini wakati sitalipa? Acheni kuuliza mambo haya nisiwapoteze bure.

            Tatu, kuanzia sasa, nitatembelea kaya nzima kuanzisha na kukagua au kufungua ‘miradi’ ya kipwagu na pwaguzi ili kuwavutia wapika kura. Katika safari na ziara zangu, lazima nimwage njuluku kama sina akili nzuri.

            Nne, nitakuwa mkarimu na mpole huku nikichanganyikana na mafyatu bila ulinzi kama ilivyokuwa kabla ya kuanza kampeni za kampani hadi waniamini na kuingia laini. Nitaingia kwenye majumba yote ya ibada na kuwamwagia mamilioni. Natoa angalizo. Mnene wa dini yeyote, orijino au feki na ya kujipachika, atakayenipinga, nampiga stopu kwa kuchanganya dini na siasa. Wajue, nitafunga maduku yao ya kuuza roho na neno. Atakayeniunga mkono na kunipigia ndogo ndogo, ruksa. Maana, huku si kuchanganya dini na siasa bali kudumisha amani na mshikamano japo kwa imani ya amani.

Tano, kila nitapozuru, lazima kutoa ahadi milioni kidogo bila kusahau kumwanga njuluku kwa wapika kura ya kula na kuwaahidi kwa kuwafyatua kuwa huo ni mwanzo tu ili wangie bila kujua kuwa, nikishaukwaa, nitawafyatua mkenge. Najua, mafyatu walivyofyatuka, watanipa. Na wakinipa, sitawapa baada ya kupewa. Watajua kuwa hawajui na wakijua hawatajua kuwa hawakujua.

            Sita, nitaanza ‘kukemea na kukoromea uoza’ ili kuwafanya mafyatu waote kuwa kaya yenye haki na tajiri kuliko zote duniani. Mfano, kila niendapo, nitatoa takwimu za kupikwa kuwaweka sawa. Nitawambia kuwa mimi ni muaminifu kuliko hata malaika na kwa Joji Kichaka na Trumpet, ndiyo maana nakopesheka.

             Saba, kwa vile sina wapinzani wa maana, nitawakandia wapingaji, ambao wengi wao wako mfukoni mwangu, kuwa hawaaminiki kama mimi japo wote, kiukweli, hatuaminiki sorry, tunaaminika. Nitawasilibia na kuwakandia kinomi. Nitasema kuwa wao wakipata ulaji, wataanza kuwatumia badala ya kuwatumikia. Watadanganya badala ya kuwaambia ukweli, kuwadhalilisha badala ya kuwaheshimu, kuwaibia badala ya kuwa waangalizi wa njuluku na mali zao.

Nitasiliba zaidi na kusema kuwa wao wanawaita funza badala ya mafyatu kiasi cha kuwaburuza badala ya kuwashawishi, kuwatesa badala ya kuwadekeza, kuwatenga badala ya kuwaunganisha.

Nane, nitaamuru magazeti yangu ya umbea kunipamba kuwa hajawahi kutokea kiongozi kama mimi tangu dunia kuumbwa. Hivyo, mafyatu wakinyima kura, wajue, wanajitia kitanzi wenyewe. Pamoja na kuwa njuluku nitakayotumia ni ya mafyatu, nitawaambia wapambe na waimba mapambio yangu waseme kuwa hii ni njuluku ya Fyatu kila ninapotoa njuluku.

Tisa, nitahubiri amani na mshikamano katika kupeana ulaji lakini si katika kula. Hivyo, yeyote anayenipinga, anapinga amani, maendeleo, na mshikamano wa mafyatu.

Kumi, nitapiga marufuku mikutano ya wapingaji na wapinzani wangu iwe ni wa wazi au kwa kificho. Nitaamuru wakubwa wa ndata za mafyatu kuvuruga mikutano ya wapingaji iwe ni kwa kuwakataza, kuwachelewesha, au kuwapa maeneo yasiyovutia ili niwapige chini kirahisi japo nao si wapingaji bali wasanii wanaotafuta ubwabwa na kutaka kuuma umma wa mafyatu. Hamjawasikia wala mafyatu wa chata la CHAKUUMA? Je wanawauma nani kama siyo mafyatu waliogeuzwa ubwabwa? Mtawaona wakidemadema na kusepasepa msijue kuwa kinachoitwa pilau si kingine bali nyinyi muhongwao udohoudoho na kuishi kwenye uchochole tokana na kughairi kufyatuka, kuendekeza tamaa, na uzwazwa hadi mkafyatuliwa kizwazwa. Nani awezaye kumvua samaki bila chambo au kwa chambo kitupu? Thubutu yako? Nioanavyo na nijuavyo, japo samaki ni hayawani, ni wajanja kuliko mafyatu wanaofyatuliwa kizwazwazwa hivi. Japo mafyatu nitakaowafyatua wanadhani wananifyatua, ukweli tutauona nikiisha ukwaa na kuanza kuwafyatua bila huruma. Nadhani hawa hawanijui uzuri.

Mwisho, nitachapisha mabango makuuuubwa tena ya mabilioni na kuyaweka kila mahali ili mafyatu wanione na kunipa. Najua. Wap viherehere wakataotaka kuhoji namna nilivyotengeza huu ukwasi na ninanunua nini. Hawa wasiwape taabu. Nitawazushia kesi kibao na kuwasweka lupango hadi mtiti uishe na kupita ndo niwaachie waendelee kupayuka huku mie nikikamua. Du! Kumbe naota!

Chanzo: Mwananchi Jana.


Faida za Kutofichana Siri na Vipato


Hakuna kitu kizuri na chenye faida na furaha kwa wanandoa kama kutofichana mambo au siri. Hapa tutaongelea athari na madhara ya kufichana kipato au kila mwanandoa kuwa na chake badala ya chetu. Wanandoa wanapokuwa wawazi kwa wenzi wao, licha ya kuwapa kuaminika na kujiamini, huwasaidia pale wanapokumbwa na misukosuko ya kifedha au kiuchumi kama vile kufilisika, kuachishwa kazi, kuugua, na mengine kama hayo. Faida nyingine ya kutoficha kipato ni kutosumbuliwa kwa kudaiwa matumizi ambayo mhusika hana uwezo nayo. Mbali na hilo, pia, hujenga kuaminiana na kushirikiana katika dhiki na raha.

            Faida nyingine ya kutokuwa na siri ni ule uhuru katika maisha ukiachia mbali kutojiruhusu kuujengea moyo wako shinikizo litokanalo na kutunza siri au uwezekano wa kufichuliwa siri. Kimsingi, siri ni kama mgando kwenye moyo (clot) wa mwenye kuiweka. Au tuseme ni moto unaounguza taratibu wenye kusababisha maumivu makali na makubwa yasiyotabirika wala kuisha. Siri ni mateso kwa mwenye kuitunza hasa siri yenyewe inapokuwa haina ulazima. Mwenye kuficha siri hana uhuru wala amani moyoni. Mwenye kutunza siri inayoweza kuivunja ndoa yake hana tofauti na mgonjwa wa kansa. Haiponi na mwisho wake ni maangamizi na misiba kwa wanandoa na familia zao. Kimsingi, mwenye kuwa na siri ana mzigo mkubwa tena unaoumiza moyo wake kila siku mbali na kumgharimu fedha, furaha, hata uhai wakati mwingine.

            Kitu kingine kinachoweza kutoa funzo na mwanga juu ya siri ni ule ukweli kuwa duniani hakuna siri tena siri ya watu wawili au zaidi. Ipo siku, kama harufu, inzi mmoja ataifichua na kuwaumbua na kuwaumiza wenye siri husika. Hii ni kutokana na ukweli kuwa binadamu hatutabiriki. Wewe unaweza kutunza siri yako. Je mwenzako au wenzako wanaweza? Kawaida, siri huvuja pale mmoja wa watunza siri anapofurahi au kuchaganyikiwa akaitoboa kwa mwingine adhaniye naye ataitunza kama yeye asijue bindamu hatutabiriki na tunabadilika. Kama serikali yenye maguvu na vyombo vyote vya usalama inatunza siri za uhai na utendaji wake, wanandoa ni nani wasifanye hivyo? Kama Mungu ametunza siri kama vile ya uumbaji na kifo, sisi ni nani tuanike siri zetu hadharani. Kwa faida gani na ya nani wakati tunajua hatari na madhara ya kufanya hivyo. Tia maanani. Dawa ya siri ni kutokuwa na siri.

Turejee kwenye kipato. Mfano, utakuta baba au mama anajali kazi yake kuliko hata ndoa! Tunakwenda wapi huko kusiko na maana wala mwelekeo? Busara haachi kuhoji hata akiitwa mkale na aliyepitwa na wakati. Ajabu, huyu ajalie kazi na kuvunja ndoa yake, akimaliza, hujikuta kazi haimtoshelezi kiasi cha kuanza kutafuta ndoa hata kwa watu wazima kuwaandama hata kuwatumia vijana wa umri wa watoto wao. Je huku si kudhalilika au kujidhalilisha?

Nani alijua kuwa ndoa inahitaji karatasi badala ya mapenzi na uaminifu? Tumeona makasisi wakizini hadi kufikishwa mahakamani. Wengine wamenajisi hadi kuuawa kwenye uchafu wao. Wengine wanaongozwa na mashoga. Je hawa na wauaji wana tofauti? Lakini bado wanatunza siri hii ambayo baadaye hufichuka na kuwaumbua na kuwaumiza. Maana, muuaji siyo auwaye mwili bali hata auawaye roho. Auwaye roho ni muuaji mbaya kuliko auawaye mwili. Mwili huoza. Nani anajua majaliwa ya roho iliyouawa na wale iliowaamini wakati hawaaminiki? Nani anajali wala kujiuliza swali kama hili? Kisu na mnafiki heri kisu maana waweza kukitahadhari. Heri mlevi umuonaye mtaani kila siku kuliko mnafiki aliyejificha kwenye utauawa au madaraka akidhani ni siri. Tusemayo siyo mapya, jipya ni kuyasema na kuyaandika.

            Tumalizie kwa kushauri na kusisitiza kuwa hakuna faida ya kuwa na siri kwa wanandoa ingawa ni vizuri kutunza siri za ndoa yao huku wakiepuka kuwa na siri nje ya ndoa yao. Siri ni mbaya na nzuri kutegemea na hiyo siri ni juu ya nini, inawahusisha nani na kwa faida gani na ya nani. Kama siri inalenga kujenga na kuimarisha ndoa, inafaa na kuswihi. Kama siri husika ni ya kubomoa ndoa, basi iepukwe mara moja.

            Mwisho, katika ndoa hakuna kazi wala mali yangu au yake bali yetu hata kama mna kazi, mali, na majukumu tofauti.

Chanzo: Mwananchi J'pili iliyopita.


Wednesday, 25 June 2025

Tunaongopa, tunaongopewa, na kuongopeana

Kuna mambo yanachusha, kukera, kutisha, kukatisha tamaa, na kusikitisha ingawa mafyatu hawatishiki japo watishwa. Tuweke sawa. Leo, nitafyatua baadhi ya mambo tufanyayo au kufanyiwa mafyatu. Mafyatu gani wasiofyatuka wakafyatua wanaowafyatua tena kirejareja kama ufjujaji na upigaje wa njuluku ndefu? Hatufyati tunapopaswa kufyatuka tukafyatua? Kuna mambo yanapaswa kudurusiwa kwa utuo ili yafanyiwe kazi lau mafyatu wanusurike na dhambi ya kujifyatua na kufyatuliwa. Je uliwahi kujiuliza kwanini tunacheka tupaswapo kununa? Je huku si kufurahia mauti yetu ya kujitakia? Je hayapo?
                 Je hatuongopi hata kuongopewa au kujiongopea tunapopaswa kusema na kuambwa ukweli? Wakweli wanachukiwa ilhali waongo wakipendwa. Wasafi wanachukiwa ilhali wachafu wakipendwa. Ni mapenzi gani haya ya hasara? Tunasifu tupaswapo kulaumu. Hatuishii hapo. Tunafurahi tunapopaswa kuchukia. Tunacheka, na kukenua, tupaswapo kununa na kulia. Tunakaa kimya tunapopaswa kupayuka. Kwanini tusifyatuliwe? Tunafyata badala ya kufyatuka! Halafu tukifyatuliwa, tunalalamika. Usipofyatuka ukafyatua, utafyatuliwa kuufyata kama si kufyata mkia. Kwa Kisambaa, huitwa the law of nature au kanuni asilia. Kazi mbi si mchezo mwema. Mjue.
                    Jiulize. Hatukubali tunapopaswa kutaa? Hatuungi mkono tupaswapo kupinga? Unapata unachotoa na kutoa unachopata. Ukipanda mbigiri, hutovuna mbirimbi. Hatupwakii tunapopaswa kususa na kutapika? Kwani, hayapo? Tunapopaswa kupoka haki, tunaiomba! Nani kakudanganya kuamini kuwa haki inaombwa na siyo kupokwa? Haki haiwezi kuwa hisani wala hisani kuwa haki. Uongo tumegeuza ukweli. Ujinga tumegeuza ujuzi. Tunaishi kwa fadhila badala ya haki. Tunaficha na kufichwa tunapopaswa kuweka wazi! Unafiki unatawala pahitajikapo kusema wazi.
Tunaogopa tunapopaswa kupambana. Tunakuwa wapole tupaswapo kuwa wakali. Tunadanganywa hadi tunajidanganya na kudanganyika mbali na kudanganyana! Je tunamdaganya nani wakati wahanga ni sisi na vizazi vyetu? Waweza kufua nguo au kuoga kwa maji machafu ukawa safi? Hamjaambwa kuwa ukiwachekea gendaeka, utavuna mabua?  Utamlaumu nani? Wangapi wanalala njaa lakini wanajiaminisha wameshiba? Wezi wanaitwa waheshimiwa ilhali watenda haki wakiitwa wanoko! Hamjayaona haya? 
            Dhuluma imegeuzwa haki. Nani hajui? Si wanasema ujanja kupata na siyo namna ulivyopata? Wangapi wanalala maskini na kuamka wakwasi huku tukiwashobokea tukiomba watuwezesha? Tuna tofauti gani na kuku hayawani aliwashaye mabaki ya mayai yake asihoji? Heri kuku ni hayawani kuliko mafyatu ambao ni waja. Kiza tunaita mwanga na mwanga kiza! Tunasema ni sawa wakati si sawa! Sawa vipi wakati mambo hayaendi sawa sawa? Penye usawa, tunabaguana. Je hatuibiani na hatubaguani kwa dini? Roho mtakatifu amekuwa roho mtakakitu na madhehebu yamegeuka maduka ya kuuza roho kwa uroho wa utajiri. 
        Ajabu, hatuwi wawazi, kusema, na kukemea! Mali ya umma inageuzwa ya wachache na wengi wanapigwa ganzi kuwa hii ni haki! Haki gani isiyo na usawa?
            Inatisha. Inaogopesha. Maskini anaitwa mwenye mali wakati yu hoi na hohehahe! Inawezekanaje fisi na mbwa wakalinda nyama au majambazi na wezi kulinda benki? Je hiki si chanzo cha ukapuku wetu? Wenye nguvu wanakula kwanza na kusaza ilhali wanyonge wakinyong’onyea hata kunyongwa na shida! Wapo wasemao eti ni haki na sawa! Kivipi? Haki vipi wakati ni dhuluma? Kwanini nisiogope na kusikitika? Je hili ni jibu au kufyatua? Heri nafyatua ili mfyatuke mfyatue, na ikibidi, tufyatuane kieleweke. Huwezi kuitwa mwenye mali wakati mali yenyewe huioni zaidi ya takwimu. Huwezi kuambwa kaya ni yako wakati ni yao. Kama ni yako, yao ni ipi, na kama ni yao, yako ni ipi? Haya ndiyo matokeo yangu kuwa fyatu mfyatuzi asiyeogopa kufyatua ili asifyatuliwe.
                Nani ataishi milele huyu mjanja tumuone? Je tumewaona wangapi wenye vifua kama ninga waliofyatuka wakaacha kila kitu wakatokomea kwenye kaburi la sahau? Mfalme aweza kuwa mfalme bila watawaliwa? Je wawili hawa nani anamhitaji au kumtegemea nani? Mbona faru na nyati huishi bila malkia wala mfalme? Nani mfalme wa ndege, viumbe huru waendao watakapo na kula watakacho japo hawazalishi? Farasi na ampandaye nani umhitaji na kumtegemea nani? Je farasi akibwaga mzigo ataumia au kupata nafuu? Mwoga na mpumbavu huogopa kifo na kuishia kufa. Si heri kupambana na adui ukafa kuliko kumuacha akudhalilishe? Heri kufa umesimama kuliko kuishi umepiga magoti. 
        Je kifo siyo faradhi? Fisi na simba hula wenzao. Je, hawauawi na kuliwa na wadudu wadogo? Tembo ana maguvu sana. Aweza kuangusha magogo kwa mamia. Je aweza kuwatisha nyuki? Pamoja na ukubwa wake, tembo huwaheshimu nyuki. Pamoja na udogo wao, koyokoyo humuua nyoka mwenye sumu kali. Je yupi bora kati ya nyoka na koyokoyo? Heri kibogoyo mwenye nyama kuliko mwenye meno asiye na nyama. Mwenye njaa asiye na chakula ni bora kuliko mgonjwa asiyeweza kula lakini akajaza chakula. Wangapi wana hamu ya kula na hawana chakula na wenye chakula hawana hamu ya kula?
            Leo, sifyatuki sana. Wala sifyati bali kuwaadhi. Hivi ni mchana au usiku?
Chanzo: Mwananchi leo.

Tuesday, 24 June 2025

Kama wakwezo wanga na wazazi wako ni wanga

Ni mara ngapi umesikia malalamiko na tuhuma za uchawi katika baadhi ya familia za wanandoa wawe wanaokuhusu au kutokuhusu? Je huwa unajisikiaje na kuelewaje? Si jambo jipya kusikia fulani akilalamika kuwa wakwe zake ni wanga. Mara nyingi, malalamiko haya hutolewa na wakamwana wanaposhindwa kuelewana na mama wakwe hata baba wake zao. Je malalamiko haya yana ukweli au ni ya kupuuza? Je ni ya kuchukulia kwa makini? Je huo wanga upo kweli au ni matokeo ya ukosefu wa sababu za msingi za kuelekea na kutatua tatizo? Je yakikuta wewe au ndugu hata rafiki, utachukua hatua gani mujarabu?

 Katika tuhuma za ‘wanga’, wengi wa watuhumiwa, au tuseme waathirika, ni mama wakwe. Baba wakwe, mara nyingi, huingizwa kwa kuunganishwa na wake zao ndipo wawe ‘wanga.’ Hata kwenye tuhuma za uchawi nje ya wanandoa, mara nyingi, wengi ni wanawake na si wanaume. Tunadhani hii ni tokana na ukaribu wa wakazamwana na mama wakwe zao. Pia, inaweza kutokana na ukweli kuwa, mara nyingi, watoto huwa karibu na mama zao kuliko baba zao japo si wote. Sababu nyingine inaweza kuwa mfumo dume unaowadhalilisha wanawake na kuwatwisha kila lawama na mizigo ya kijamii.

          Hata hivyo, wakati tukidurusu na kutafakari dhana nzima ya wanga, tujiulize maswali kadhaa:

          Je kweli wakwe wanaotuhumiwa ni wanga kweli au mwanga ni yule anayewatuhumu? Je wanga unaweza kuthibitishwa kisayansi? Kisheria, tunajua wazi, wanga hauwezi kuthibitishwa. Ni matokeo ya ujinga na imani za hovyo. Je ni kweli wanga upo na wahusika wanaufanya? Ili iweje?

Tukiangalia tuhuma za wanga dhidi ya wake, kuna baadhi ya maswali ya ziada ya kujiuliza. Je ilikuwaje, kama kweli ni wanga, waliweza kumlea huyo mumeo hadi akakua na kukuoa wasimuwangie hata kumua? Je angakuwa mama yako au wazazi wako wote ndiyo wanaotuhumiwa wanga na mwenzi wako ungefanya nini?

Katika kudurusu na kuchunguza dhana hizi za kijinga zitokanazo na chuki na ukosefu wa umakini katika kuendea matatizo, tunapendekeza hatua zifuatazo kuchukuliwa ili kuepusha kusambaratisha ndoa hata jamii.

Mosi, ni vizuri kwa wanandoa kujielimisha juu ya dhana nzima ya uwanga na sababu za kuwepo kwake ziwe za kweli, uongo, chuki, hata kisayansi. Hii ni kutokana na ukweli kuwa dhana hizi zipo. Hivyo, haziwezi kufumbiwa macho hasa ikizingatiwa kuwa madhara yake huwa mabaya na makubwa.

Pili, wanandoa waepuke chuki na dhana potofu ambazo nazo huchangia sana uwepo wa dhana hizi mbovu. Baya zaidi, wahusika wanaposhindwa kutumia akili kutatua tatizo ambalo laweza kwa chuki binafsi, uchoyo, hata umaskini, hupanua wigo wa tatizo kwa kuhusisha wapiga ramli, wachungaji, na hata mashoga ambao huongeza hatari kwa wanandoa na familia zao.  

        Mfano, muathirika anaweza kwenda kwa mganga wa kienyeji au mchungaji ili kuaguliwa, kuzindikwa, hata kuombewa bila kujua kuwa hao anaowapelekea matatizo yake, wakati mwingine, wanakuwa na matatizo makubwa kuliko yake.

Tatu, jamii inapaswa kuachana na unyanyasaji wa kijinsia ambapo waathirika wakubwa huwa ni wanawake zaidi ya wanaume. Katika utafiti aliofanya Daktari Philippa Carter, mwaka 2023, aligundua kuwa huko Marekani na Uingereza, kulikuwa na visa vya tuhuma za uchawi.                             Watuhumiwa wote walikuwa 802 kulingana na rekodi za mpiga ramli maarufu wa Uingereza Richard Nappier (1559-1 April 1634) na kugundua kuwa kati ya watuhumiwa hao, 500 walikuwa wanawake na wanaume 232 ambapo malalamiko 70 hayakuwa yameorodheshwa. Katika kitabu chake  Malleus Malleficarum (2023), mwandishi Heinrich Kramer alibaini kuwa, kutokana na kuwa hadhi ya chini ikilinganishwa na wanaume, ni chanzo kikubwa cha kutuhumiwa uchawi.

Nne, tunashauri kuwa kabla ya kuwashutumu wengine, jiweke kwenye viatu vyao na kufikiri nje ya boksi. Je utajisikiaje kama wifi yako atawatuhumu wazazi wako kuwa wanga wakati unajua si wanga bali chuki na hila tu? Je utakapozeeka, likikutokea hili, utajisikiaje? Japo hili hulioni, kwa namna ulivyo mnyama, Mungu lazima atakulipa. Kwani malipo ni hapa hapa. Usishangae yakakukuta haya unayowafanyia wenzako tena bila sababu yoyote bali ujinga, roho mbaya, uroho, na kushindwa kufikiri sawa sawa.


Wednesday, 18 June 2025

Mnaringia ‘kiinglish’ are you British or Brutish!!


 Juzi nilishuhudia vita ya kikumbaff na kizwazwa ya mafyatu, au niseme uchangudoa wa kimaadili, ushamba wa kiakili, na ulimbuekeni wa kitabia. Si baada ya mafyatu wa haki za mafyatu kutoka kaya jirani kwenda kusikiliza mtiti wa fyatu mwenzao aliyetaka kukinukisha ili wote wanuke. Walizuiliwa kizembe na kuregeshwa makwao wengine wakiwa hai japo hoi. Kwa sababu wanadai walifanyiwa kitu mbaya bila hata kutoa ushahidi. 

                Acha mafyatu wafyatuane na kuvuana nguo hadharani tena mchana kutwa wakati wenye ngoma yao ni wanene. Badala ya kuwafyatua wanene waliowafyatua wenzao, waliingia ntego na kuanza kufyatuana wenyewe kwa wenyewe. Kwanini mnacheza ngoma ya wengine mkidhani yenu nyambaff wakubwa? Mitusi mizito mizito ilianza kurushwa toka upande zote. Watukufu walitukanwa hadi kikanukishwa kifyatu.

            Nani angeamini kuwa na waishiwa toka pande zote wangetia timu kwenye huu ukumbaff? Walipoteza hata muda wa buge kwa ubugeubuge kama huu! Ukiachia mitusi husika kuhuzunisha na kushangaza, hakuna kilichonishangaza hadi nikaamua kufyatua hili onyo na suto tena kwa Kiswahili japo nshafyatua kwa kiinglish wiki mbili zilizopita. Katika kujitahidi kubagazana na kubaguana, mafyatu wa upande wa pili walishikilia uzwazwa mmoja. 

                Kila wakirusha mikombora ya mitusi, utasikia “nyinyi hamujui kiingeredha.” Kwanza, inshu ilikuwa ni nani anakimanya kibritish au kufyatuliwa haki za binadamu za mafyatu kama kuwekwa tunduni na kupiga persona non grata? Je hii ni nini? Rudi darasani ukasome. Kwa tuliowahi kuishi Kenya, wanaowatuhumu wenzao kutokijua kimombo aka kithungu au kithunguri, wao ndiyo usiseme. Hawakijui wala Kiswahili.

  Hapa naongea na akina Kariuki wa Muriuki au mfufuka aka Karish, Njoroge aka Njoro, Shiko, Waruguru, Khalwale, Awori, Sifuna, Wanyonyi, Ocholla, Omoro, Amoro, Maboi, na wengine wengi. Mwenzenu niliishi maeneo ya Valley Arcade kule Lavington kwa wanene. Hivyo, nawajua kuliko hata mnavyowajua wabongo wenzangu.

            Namaanisha akina Onyango Oburu wajiitao Mc Onyango. Hata mujiite Mac Donald bado ni manugu tu. Wengine wanajiita Doug badala ya Douglas. Si mujiite dog au mbwa ijulikane kama siyo ngui. Kwani nyinyi ni waingereza? Wathunguri au wadhungu wakiwadharau mnalaumu. Basi, badilisheni rangi muwe hao wathunguri. 

                Mbona kama ni kiingirish ni mali mbona mwapeleka vitegemezi vyenu kwa Bro M7 na kitegemezi chake the Avenger aka Muhoooooziiii kohooziiiii ziii? Sijui kama na waiingilish wanajivunia Kijaluo, Kikikuyu hata Kikamba ya kana ka mkamba wa Kaneza, Wamuseto na Wakaiti. Eti Wabongo hawajui Kiingereza. Kwani, nyinyi ni wabritish. Kama watawaona kama manyani, mtaanza kulalamika eti mnabaguliwa? Kumbe mfalme Charles ana koloni ambalo amelisahau la Black Brits. Great minds speak bout ideas, avarage minds discuss events, and small minds discuss people.

            Tokana na mitusi hiyo hapo juu, sijui uhuru wenu unamaanisha nini hadi mnajisifia kibritish wakati Wainglish wanawaona nyinyi ni brutish tuu tena weusi wanaobaguliwa na hao mabritish mnaowaramba makalio? Mbona hamli vyakula vya kibritish bali kathubu kanini, kamceri, makande, mutula, mukimo, madodo na kadhalika? Kabla ya kusema Wabongo hawajui kimombo, nenda kawasilikize akina Mvaithe. Utasikia fyatu akisema, nthis is nthe mbrother from my nconsitituency.  Ukija kwa akina Njoro, utasikia this is mokey business au idepedece yaani uhuru. Shame on you! It is time to stop self-dressing down now.

Acheni jamani. Wenye akili wanawacheka mnavyopwakia na kujivunia lugha za watu.

            Nilisikia wakidai kuwa Bongo bila Kenya haiwezi kuishi na pia ni maskini wakati ukweli ni tofauti. Mnamaanisha Kenya na Bongo ipi? Mnadhani hao waTZ hawawajui uzuri siyo? Mmenoeni tena sana. Wajua muishivyo kwa shida mazee. Nenda Kibera halafu urudi bongo ulinganishe na sehemu yoyote Uswekani. Wengi huwa tunasema eti Manzese ni uswekeni. Jamanini, nendeni Kawangware au ngwaro, Kibera aka kibra,  Mukuru kwa Njenga (wao husema Jenga), Kiandutu (cha funza), Korogocho, Muthurwa, nk. Msipigwe chenga la mato. Nendeni muone halafu mjue mnatukanwa na mafyatu gani.

                 Uliona wapi Bongo fyatu anapanga nyumba bila choo huku akiambiwa choo siyo sehemu ya nyumba? Je huwa wanafanyaje? Jikumbushe kipindi fulani pale jamaa zetu toka kule gabacho..rii walivyoanza kutumia kitu ambacho kwa wenzetu hujulikana kama flying toilets. Fyatu zima sijui na mke na watoi linajisikia kwenda kutua mzigo, linafungua mfuko wa plastiki na kumalizia mambo humo na kurusha mtaani. Hawa ndiyo wabrutish wetu wanaokimanya kibritish japo siyo wote.

            Sasa jiulize nani kapuku. Mwaka 2023, hao wajivuni walituuzia bidhaa zisozidi dolari milioni 14 wakati sisi tukiwauzia bidhaa zenye thamani ya dolari miloni 178 nyingi zikiwa vyakula wakati wao walituuzia bidhaa za viwandani. Ukienda mbele, wanachoringia kutuzidi GDP, utakuta mali nyingi inamilikiwa na watasha na magabacholi.

             Japo nasi tuna tatizo hilo, tunawazidi kitu kimoja. Hatuna wapangaji vijijini kama hawa jamaa ambao huishi kwenye reserves kama waanimo tena kwenye nyumba za mabati kama magari. Nyani angeona nonihino lake, bila shaka, asingewacheka wenzake. Ni ajabu nyani kumcheka mbuzi ambaye nonihino lake limefunikwa na mkia japo wote ni waanimo. Du! Hii mibangi!

Chanzo: Mwananchi leo.